Luka 18 - Swahili Revised Union Version

Mfano wa mjane na hakimu

1 Rum 12:12; Kol 4:2; 1 The 5:17 Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.

2Akasema, Palikuwa na hakimu katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu.

3Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendeaendea, akisema, Nipatie haki na adui wangu.

4Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu,

5Lk 11:7,8 lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima.

6Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule hakimu dhalimu.

7Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?

8Nawaambia, atawapatia haki upesi; lakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?

Mfano wa Farisayo na mtoza ushuru

9Akawaambia mfano huu watu waliojiamini ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote.

10Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru.

11Isa 58:2,3; Lk 16:15 Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.

12Mt 23:23 Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote.

13Zab 51:1 Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipigapiga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.

14Mt 23:12; Lk 14:11; Eze 21:31 Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.

Yesu awabariki watoto wadogo

15 Mt 19:13-15; Mk 10:13-16 Wakamletea na watoto wachanga ili awaguse; lakini wanafunzi walipoona waliwakemea.

16Bali Yesu akawaita waje kwake, akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa kuwa watu kama hao ufalme wa Mungu ni wao.

17Mt 18:3 Amin, nawaambia, Mtu yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hauingii kamwe.

Mtawala tajiri

18 Mt 19:16-29; Mk 10:17-30 Tena, mtawala mmoja alimwuliza, akisema, Mwalimu mwema, nifanye nini ili nipate kuurithi uzima wa milele?

19Yesu akamwambia, Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, naye ndiye Mungu.

20Kut 20:12-16; Kum 5:16-20 Wazijua amri; Usizini, Usiue, Usiibe, Usishuhudie uongo, Waheshimu baba yako na mama yako.

21Akasema, Hayo yote nimeyashika tangu utoto wangu.

22Mt 6:20 Yesu aliposikia hayo alimwambia, Umepungukiwa na neno moja bado; viuze ulivyo navyo vyote, ukawagawie maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha, njoo unifuate.

23Lakini aliposikia hayo alihuzunika sana, maana alikuwa na mali nyingi.

24Yesu alipoona vile alisema, Kwa shida gani wenye mali watauingia ufalme wa Mungu!

25Kwa maana ni rahisi ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.

26Nao waliosikia walisema, Ni nani basi awezaye kuokoka?

27Akasema, Yasiyowezekana kwa wanadamu yawezekana kwa Mungu.

28Petro akasema, Tazama, sisi tumeviacha vitu vyetu vyote na kukufuata.

29Akawaambia, Hakika nawaambia, hakuna mtu aliyeacha nyumba, au mke, au ndugu, au wazazi, au wana, kwa ajili ya ufalme wa Mungu,

30asiyepokea zaidi mara nyingi katika wakati huu, na katika ulimwengu ujao uzima wa milele.

Yesu atabiri kuhusu kufa na kufufuka kwake kwa mara ya tatu

31 Mt 20:17-19; Mk 10:32-34 Akawachukua wale Kumi na Wawili, akawaambia, Tazameni, tunapanda kwenda Yerusalemu, na mambo yote, Mwana wa Adamu aliyoandikiwa na manabii yatatimizwa. Lk 9:22,44

32Kwa kuwa atatiwa mikononi mwa Mataifa, atafanyiwa dhihaka; atatendwa jeuri, na kutemewa mate;

33nao watampiga mijeledi, kisha watamwua; na siku ya tatu atafufuka.

34Mk 9:32 Lakini hawakuelewa maneno hayo hata kidogo, na jambo hilo lilikuwa limefichwa kwao, wala hawakufahamu yaliyonenwa.

Yesu amponya mwombaji kipofu

35 Mt 20:29-34; Mk 10:46-52 Ikawa alipokaribia Yeriko, mtu mmoja kipofu alikuwa ameketi kando ya njia, akiomba sadaka;

36na alipowasikia makutano wakipita, aliuliza, Kuna nini?

37Wakamwambia, Yesu wa Nazareti anapita.

38Akapiga kelele, akisema, Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu.

39Basi wale waliotangulia wakamkemea ili anyamaze; lakini yeye alizidi sana kupaza sauti, Ee Mwana wa Daudi, unirehemu.

40Yesu akasimama, akaamuru aletwe kwake; na alipomkaribia, alimwuliza,

41Unataka nikufanyie nini? Akasema, Bwana, nipate kuona.

42Lk 17:19 Yesu akamwambia, Upewe kuona; imani yako imekuponya.

43Mara hiyo akapata kuona, akamfuata, huku akimtukuza Mungu. Na watu wote walipoona hayo walimsifu Mungu.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help