Mhubiri 12 - Swahili, Common Language Bible with DCs

1Umkumbuke Muumba wako siku za ujana wako,

kabla hazijaja siku na miaka ambapo utasema:

“Sifurahii tena vitu hivyo!”

2 Umkumbuke kabla ya wakati ambapo kwako mwanga wa jua utafifia;

mwezi na nyota haviangazi tena,

nayo mawingu yametanda tena baada ya mvua.

3Wakati ambapo mikono inayokulinda inatetemeka,

miguu yako imara imepindika,

meno yako ya kusagia hayafai kwa uchache,

na macho ya kuchungulia dirishani yamefifia.

4Wakati ambapo milango ya masikio yako imezibika,

na sauti za visagio ni hafifu;

lakini usiku hata kwa sauti ya ndege utagutuka.

5Wakati huo utaogopa kupanda mahali pa juu

na kutembea barabarani ni kitisho;

wakati miti ya mlozi inachanua na panzi wanashiba,

lakini wewe hutakuwa na hamu tena.

Wakati huo binadamu anapaswa kwenda katika makao yake ya milele,

nao waombolezaji watapitapita barabarani.

6Wakati huo uzi wa dhahabu utakatika,

bakuli la dhahabu litapasuka,

mtungi wa maji utavunjikia kisimani,

kadhalika na gurudumu la kuvutia maji.

7Nawe vumbi utarudia udongoni ulimotolewa

na roho yako itamrudia Mungu aliyeiumba.

8Mimi Mhubiri nasema: Yote ni bure kabisa! Yote ni bure.

Hatima

9Basi, zaidi ya kuwa na hekima yake, Mhubiri aliwafundisha watu ujuzi. Alizipima, akazichunguza na kuzirekebisha methali kwa ustadi mwingi.

10Mhubiri alijitahidi kupata maneno ya kupendeza, akaandika kwa ufasaha maneno ya kweli.

11Misemo ya wenye hekima ni kama michokoo na methali zilizokusanywa pamoja na mchungaji mmoja ni kama vigingi vilivyopigiliwa imara ardhini.

12Zaidi ya hayo, mwanangu, jihadhari! Kuandika vitabu hakuna mwisho na kusoma kwingi huchokesha mwili.

13Baada ya hayo yote yaliyokwisha semwa bado kuna hili linalotakiwa: Mche Mungu, na uzishike amri zake; kwa sababu hilo ndilo jukumu aliloumbiwa binadamu.

14Maana, Mungu atahukumu matendo yetu yote, hata yale yanayotendwa kwa siri, yawe mema au mabaya.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help