Yobu 17 - Swahili, Common Language Bible with DCs

1“Nimevunjika moyo, siku zangu zimekwisha,

kaburi langu liko tayari.

2Kweli wanaonidhihaki wamenizunguka,

dhihaka zao naziona dhahiri.

3“Ee Mungu, uwe mdhamini wangu mbele yako,

maana hakuna mwingine wa kunidhamini.

4Maadamu umezifumba akili za rafiki zangu;

usiwaache basi wanishinde.

5Mtu anayewasaliti rafiki zake kwa faida

watoto wake watakufa macho.

6“Nimefanywa kuwa kichekesho kwa watu

nimekuwa mtu wa kutemewa mate.

7Macho yangu yamefifia kwa uchungu;

viungo vyangu vyote vimekuwa kama kivuli.

8Wanyofu wanaduwaa waonapo balaa langu,

nao wasio na hatia hujichochea

dhidi ya mtu wanayedhani hamchi Mungu.

9Hata hivyo, mnyofu hushikilia msimamo wake,

mtu atendaye mema huzidi kuwa na nguvu zaidi.

10Lakini nyinyi njoni, njoni nyote tena,

kwenu sitampata mwenye hekima hata mmoja.

11“Siku zangu zimekwisha, mipango yangu imevunjwa;

matazamio ya moyo wangu yametoweka.

12Kwa hao rafiki zangu usiku ni mchana;

je, ndio kusema mna mwanga gizani humu?

13Kwa vile Kuzimu ndio nyumba yangu,

na makao yangu yamo humo gizani;

14kama naliita kaburi ‘baba yangu’

na buu, ‘mama yangu’ au ‘dada yangu’,

15je, nimebakiwa na tumaini gani?

Ni nani awezaye kuona tumaini hilo?

16Tazamio langu litashuka nami kuzimu!

Tutateremka sote wawili hadi huko mavumbini!”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help