Zaburi 41 - Swahili, Common Language Bible with DCs

Sala ya mgonjwa(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi)

1Heri mtu anayewajali maskini;

Mwenyezi-Mungu atamwokoa wakati wa shida.

2Mwenyezi-Mungu atamlinda na kumweka hai,

naye atafanikiwa katika nchi;

Mungu hatamwacha makuchani mwa maadui zake.

3Mwenyezi-Mungu atamsaidia awapo mgonjwa,

atamponya maradhi yake yote.

4Nami nilisema: “Unifadhili, ee Mwenyezi-Mungu,

unihurumie maana nimekukosea wewe.”

5Madui zangu husema vibaya juu yangu:

“Atakufa lini na jina lake litoweke!”

6Wanitembeleapo husema maneno matupu;

wanakusanya mabaya juu yangu,

na wafikapo nje huwatangazia wengine.

7Wote wanichukiao hunongonezana juu yangu;

wananiwazia mabaya ya kunidhuru.

8Husema: “Maradhi haya yatamuua;

hatatoka tena kitandani mwake!”

9 Taz Mat 26:23; Marko 14:18; Luka 22:21; Yoh 13:18 Hata rafiki yangu wa moyoni niliyemwamini,

rafiki ambaye alishiriki chakula changu,

amegeuka kunishambulia!

10Ee Mwenyezi-Mungu, unionee huruma!

Unipe nafuu, nami nitawalipiza.

11Hivyo nitajua kwamba unapendezwa nami,

maadui zangu wasipopata fahari juu yangu.

12Wewe umenitegemeza kwani natenda mema;

waniweka mbele yako milele.

13 Taz Zab 106:48 Asifiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli,

tangu milele na hata milele!

Amina! Amina!

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help