Zaburi 79 - Swahili, Common Language Bible with DCs

Wakati wa maafa ya taifa(Zaburi ya Asafu)

1Ee Mungu, watu wasiokujua wameivamia nchi yako.

Wamelitia najisi hekalu lako takatifu,

na kuufanya mji wa Yerusalemu kuwa magofu.

2Wameacha maiti za watumishi wako ziliwe na ndege,

miili ya watu wako chakula cha wanyama wa porini.

3Damu yao imemwagwa kama maji mjini Yerusalemu,

wamelazwa humo na hakuna wa kuwazika.

4Tumekuwa aibu kwa mataifa ya jirani,

jirani zetu wanatucheka na kutudhihaki.

5Ee Mwenyezi-Mungu, je, utakasirika hata milele?

Hasira yako ya wivu itawaka kama moto hata lini?

6Uwamwagie watu wasiokujua hasira yako;

naam, tawala zote zisizoheshimu jina lako.

7Maana wamemmeza Yakobo, taifa lako,

wameteketeza kabisa makao yake.

8Usituadhibu kwa sababu ya makosa ya wazee wetu.

Huruma yako itujie haraka,

maana tumekandamizwa mno!

9Utusaidie, ee Mungu, mwokozi wetu;

kwa heshima ya jina lako

utuokoe na kutusamehe dhambi zetu,

kwa ajili ya jina lako.

10Kwa nini mataifa yatuambie:

“Yuko wapi Mungu wenu?”

Utujalie tuone ukiwalipiza watu wa mataifa

mauaji ya watumishi wako.

11Kilio cha hao wafungwa kikufikie;

kwa nguvu yako kuu uwaokoe waliohukumiwa kufa.

12Mataifa hayo yaliyokudharau, ee Bwana,

yalipizwe mara saba!

13Nasi watu wako, tulio kondoo wa kundi lako,

tutakushukuru milele,

na kukusifu nyakati zote.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help