Hosea 8 - Kiswahili Study Bible

Makosa makuu ya Israeli

1“Pigeni baragumu!

Adui anakuja kama tai

kuivamia nyumba ya Mwenyezi-Mungu,

kwa kuwa wamelivunja agano langu

na kuiasi sheria yangu.

2Waisraeli hunililia wakisema:

‘Mungu wetu, sisi tunakujua.’

3Lakini Israeli amepuuza mambo mema,

kwa hiyo, sasa adui watamfuatia.

4“Walijiwekea wafalme bila kibali changu,

walijiteulia viongozi ambao sikuwatambua.

Wamejitengenezea miungu ya fedha na dhahabu,

jambo ambalo litawaangamiza.

5Watu wa Samaria, naichukia sanamu yenu ya ndama.

Hasira yangu inawaka dhidi yenu.

Mtaendelea mpaka lini kuwa na hatia?

6Nanyi Waisraeli ni hivyohivyo!

Na sanamu yenu hiyo fundi ndiye aliyeitengeneza.

Yenyewe si Mungu hata kidogo.

Naam! Sanamu ya ndama ya Samaria itavunjwavunjwa!

7“Wanapanda upepo, watavuna kimbunga!

Mimea yao ya nafaka iliyo mashambani

haitatoa nafaka yoyote.

Na hata kama ikizaa,

mazao yake yataliwa na wageni.

8Waisraeli wamemezwa;

sasa wamo kati ya mataifa mengine,

kama chombo kisicho na faida yoyote;

9kwa kuwa wamekwenda kuomba msaada Ashuru.

Efraimu ni punda anayetangatanga peke yake;

Efraimu amekodisha wapenzi wake.

10Wametafuta wapenzi kati ya watu wa mataifa,

lakini mimi nitawakusanya mara.

Na hapo watasikia uzito wa mzigo,

ambao mfalme wa wakuu aliwatwika.

11“Watu wa Efraimu wamejijengea madhabahu nyingi,

na madhabahu hizo zimewazidishia dhambi.

12Hata kama ningewaandikia sheria zangu mara nyingi,

wao wangeziona kuwa kitu cha kigeni tu.

13Wanapenda kutoa tambiko,

na kula nyama yake;

lakini mimi Mwenyezi-Mungu sipendezwi hata kidogo.

Mimi nayakumbuka makosa yao;

nitawaadhibu kwa dhambi zao;

nitawarudisha utumwani Misri.

14Waisraeli wamemsahau Muumba wao,

wakajijengea majumba ya fahari;

watu wa Yuda wamejiongezea miji ya ngome,

lakini mimi nitaipelekea moto miji hiyo,

na kuziteketeza ngome zao.”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help