Zaburi 74 - Kiswahili Study Bible

Ombolezo juu ya kubomolewa hekalu(Utenzi wa Asafu)

1Kwa nini, ee Mungu, umetutupa kabisa?

Mbona hasira yako inawaka dhidi ya kondoo wako!

2Kumbuka jumuiya yako uliyojipatia tangu kale,

kabila ulilolikomboa liwe mali yako,

kumbuka mlima Siyoni mahali unapokaa.

3Pita juu ya magofu haya ya kudumu!

Adui wameharibu kila kitu hekaluni.

4Maadui zako wamenguruma ushindi hekaluni mwako!

Wameweka humo bendera zao za ushindi!

5Wanafanana na mtema kuni,

anayekata miti kwa shoka lake.

6Waliivunjavunja milango ya hekalu,

kwa mashoka na nyundo zao.

7Walichoma moto patakatifu pako;

walikufuru mahali pale unapoheshimiwa.

8Walipania kutuangamiza sote pamoja;

walichoma kila mahali tulipokutania kukuabudu nchini.

9Hatuzioni tena ishara zetu takatifu,

hatuna tena nabii yeyote!

Hata hatujui yatakuwa hivi hadi lini!

10Mpaka lini, ee Mungu, adui atakucheka?

Je, watalikufuru jina lako milele?

11Mbona umeuficha mkono wako?

Kwa nini hunyoshi mkono wako?

12Hata hivyo wewe Mungu ni mfalme wetu tangu kale;

umefanya makuu ya wokovu katika nchi.

13Kwa enzi yako kuu uliigawa bahari;

uliviponda vichwa vya majoka ya bahari.

14Wewe uliviponda vichwa vya dude Lewiyathani;

ukawapa wanyama wa jangwani mzoga wake.

15Wewe umefanya chemchemi na vijito;

na kuikausha mito mikubwa.

16Mchana ni wako na usiku ni wako;

umeweka mwezi na jua mahali pao.

17Wewe umeweka mipaka yote ya dunia;

umepanga majira ya kiangazi na ya baridi.

18Kumbuka, ee Mwenyezi-Mungu, madharau ya maadui zako;

taifa pumbavu linalikashifu jina lako.

Sisi ni dhaifu kama njiwa.

19Usiwatupie wanyama wakali uhai wa wapenzi wako;

usiyasahau maisha ya maskini wako.

20Ulikumbuke agano ulilofanya nasi!

Nchi imejaa uharamia kila mahali pa giza.

21Usiwaache wanaokandamizwa waaibishwe,

uwajalie maskini na wahitaji walisifu jina lako.

22Inuka, ee Mungu, ukajitetee;

ukumbuke wanavyokudharau kila siku watu wasiokujua.

23Usisahau makelele za maadui zako;

na ghasia za daima za wapinzani wako.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help