Zaburi 115 - Kiswahili Study Bible

Mungu mmoja wa kweli

1Sio sisi, ee Mwenyezi-Mungu, sio sisi;

bali wewe peke yako utukuzwe,

kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako.

2Kwa nini mataifa yaseme:

“Mungu wenu yuko wapi?”

3Mungu wetu yuko mbinguni;

yeye hufanya yote anayotaka.

4Miungu yao ni ya fedha na dhahabu;

imetengenezwa kwa mikono ya wanadamu.

5Ina vinywa, lakini haisemi.

Ina macho, lakini haioni.

6Ina masikio, lakini haisikii.

Ina pua, lakini hainusi.

7Ina mikono, lakini haipapasi.

Ina miguu, lakini haitembei.

Haiwezi kamwe kutoa sauti.

8Wote wanaoitengeneza wanafanana nayo,

kadhalika na wote wanaoitumainia.

9Enyi Waisraeli, mtumainieni Mwenyezi-Mungu;

yeye ndiye msaada wenu na ngao yenu.

10Enyi wazawa wa Aroni, mtumainieni Mwenyezi-Mungu;

yeye ndiye msaada wenu na ngao yenu.

11Enyi mnaomcha Mwenyezi-Mungu, mtumainini,

yeye ndiye msaada wenu na ngao yenu.

12Mwenyezi-Mungu atukumbuka na atatubariki;

atawabariki watu wa Israeli,

atawabariki wazawa wa Aroni.

13Atawabariki wote wamchao,

atawabariki wakubwa na wadogo.

14Mwenyezi-Mungu awajalieni muongezeke;

awajalieni muongezeke nyinyi na wazawa wenu!

15Mbarikiwe na Mwenyezi-Mungu,

aliyeziumba mbingu na dunia.

16Mbingu ni mali yake Mwenyezi-Mungu,

bali dunia amewapa binadamu.

17Wafu hawamsifu Mwenyezi-Mungu,

wala wale wanaoshuka katika nchi ya kimya.

18Lakini sisi tulio hai twamsifu Mwenyezi-Mungu;

tutamsifu sasa na hata milele.

Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help