1“Binadamu anayo magumu duniani,
na siku zake ni kama siku za kibarua!
2Yeye ni kama mtumwa atamaniye kivuli,
kama mwajiriwa angojaye kwa hamu mshahara wake.
3Basi nimepangiwa miezi na miezi ya ubatili,
yangu ni majonzi usiku hata usiku.
4Nilalapo nasema, ‘Nitaamka lini?’
Kwani saa za usiku huwa ndefu sana;
nagaagaa kitandani mpaka kuche!
5Mwili wangu umejaa mabuu na uchafu;
ngozi yangu imekauka na kutokwa na usaha wa jipu.
6Siku zangu zapita kasi kuliko gurudumu la mshonaji,
nazo zafikia mwisho wake bila matumaini.
7“Kumbuka, maisha yangu ni pumzi tu;
jicho langu halitaona jema lolote tena.
8Anayeniona sasa, hataniona tena,
punde tu ukinitazama nitakuwa nimetoweka.
9Kama wingu lififiavyo na kutoweka
ndivyo nao watu washukavyo kuzimu bila kurudi.
10Anayeondoka harudi tena kwa jamaa yake,
na pale alipokuwa anaishi husahaulika mara.
11“Kwa hiyo sitakizuia kinywa changu kuongea;
nitasema kwa msongo wa roho yangu,
nitalalamika kwa uchungu wa nafsi yangu.
12Je, mimi ni bahari au dude la baharini
hata uniwekee mlinzi?
13Nikisema, ‘Kitanda kitanipumzisha,
malazi yangu yatanipunguzia malalamiko yangu,’
14wewe waja kunitia hofu kwa ndoto,
wanitisha kwa kuniletea maono;
15hata naona afadhali kujinyonga,
naona heri kufa kuliko kupata mateso haya.
16Nayachukia maisha yangu;
sitaishi milele.
Niacheni, maana siku zangu ni pumzi tu!
17Binadamu ni nini hata umjali?
Kwa nini hata unajishughulisha naye?
18Wewe waja kumchunguza kila asubuhi,
kila wakati wafika kumjaribu!
19Utaendelea kuniangalia hata lini,
bila kuniacha hata nimeze mate?
20Kama nikitenda dhambi,
yakudhuru nini ewe mkaguzi wa binadamu?
Mbona umeniweka kuwa shabaha ya mapigo yako?
Je, mimi nimekuwa mzigo kwako?
21Mbona hunisamehi kosa langu
na kuniondolea uovu wangu?
Hivi punde nitalazwa chini kaburini,
utanitafuta, lakini sitakuwapo tena!”
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.