1Basi, Mose akawaambia Waisraeli kila kitu kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru.
Mwongozo kuhusu nadhiri2
3“Mtu akiweka nadhiri kwa Mwenyezi-Mungu au akiahidi kwa kiapo na kujifunga nafsi yake kwa ahadi, ni lazima atimize ahadi yake; ni lazima atekeleze yote yale aliyotamka kwa kauli yake.
4“Msichana ambaye bado anaishi nyumbani kwa baba yake akiweka nadhiri kwa Mwenyezi-Mungu na kujifunga mwenyewe kwa ahadi,
5na baba yake akawa amesikia ahadi hiyo, asimpinge, basi, nadhiri zake alizoweka zitambana na kila ahadi aliyotoa itambana.
6Lakini kama baba yake akisikia juu ya nadhiri hiyo, akampinga, basi nadhiri zake na ahadi yake havitambana. Mwenyezi-Mungu atamsamehe kwa sababu baba yake amelipinga jambo hilo.
7“Ikiwa msichana ataolewa baada ya kuweka nadhiri, au kuahidi bila ya kufikiri vizuri kwanza, na akajifunga mwenyewe,
8halafu mumewe akasikia jambo hilo asimpinge, basi nadhiri zake zitambana na ahadi zake zitambana.
9Lakini kama mume wake akisikia jambo hilo akampinga, basi huyo mumewe atabatilisha nadhiri ya mkewe na tamko lake alilotoa bila kufikiri; naye Mwenyezi-Mungu atamsamehe.
10“Lakini nadhiri au ahadi yoyote aliyoiweka mama mjane au mwanamke aliyepewa talaka ambayo kwayo amejifunga, ni lazima imbane.
11“Mwanamke aliyeolewa akiweka nadhiri au akiahidi kwa kiapo akiwa nyumbani kwa mumewe,
12kisha mume wake akasikia jambo hilo lakini asimpinge, wala kumwambia kitu, basi, nadhiri zake zote zitambana; kadhalika na ahadi zake zote zitambana.
13Lakini kama mumewe atakaposikia habari zake, akizitangua na kuzibatilisha, basi, hata kama alitaka kutimiza nadhiri au ahadi zake, hatawajibika kuzitimiza; mumewe atakuwa amezitangua na Mwenyezi-Mungu atamsamehe.
14Mumewe anaweza kuthibitisha au kutangua nadhiri au ahadi yoyote inayomfunga.
15Lakini ikiwa mumewe hatasema neno lolote tangu siku atakaposikia habari za nadhiri au ahadi za mkewe, basi atakuwa amezithibitisha siku hiyo alipopata habari zake kwa sababu hakusema chochote.
16Lakini akizibatilisha na kuzitangua muda fulani baada ya kusikia habari zake, basi yeye atakuwa na lawama kwa kosa la mkewe.”
17Hizi ndizo kanuni ambazo Mwenyezi-Mungu alimwagiza Mose juu ya mume na mkewe; baba na binti yake, huyo binti akiwa bado kijana na anakaa nyumbani kwa baba yake.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.