Isaya 39 - Kiswahili Study Bible

Wajumbe kutoka Babuloni(2 Fal 20:12-19)

1Wakati huo, mfalme Merodak-baladani mwana wa Baladani, mfalme wa Babuloni, aliposikia kwamba Hezekia alikuwa ameugua na sasa amepona, alimtumia ujumbe pamoja na zawadi.

2Basi, Hezekia aliwakaribisha na kuwaonesha nyumba ya hazina: fedha, dhahabu, viungo vya kukolezea chakula, mafuta ya thamani, vifaa vyake vyote vya kijeshi na vitu vyote vilivyokuwamo katika bohari zake. Hakuna chochote katika ikulu yake au katika nchi yake ambacho hakuwaonesha.

3Ndipo nabii Isaya alipokwenda kwa mfalme Hezekia na kumwuliza, “Watu hawa wamesema nini? Na, wamekujia kutoka wapi?” Naye Hezekia akamjibu “Wamenijia kutoka nchi ya mbali, huko Babuloni.”

4Halafu Isaya akamwuliza, “Wameona nini katika ikulu yako?” Hezekia akamjibu, “Wameona yote yaliyomo katika ikulu yangu. Hakuna chochote katika bohari zangu ambacho sikuwaonesha.”

5Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la Mwenyezi-Mungu wa majeshi:

6Tazama, siku zinakuja ambapo vyote vilivyomo nyumbani mwako na vitu vyote walivyokusanya wazee wako hadi leo, vitapelekwa mpaka Babuloni. Hakuna kitu chochote kitakachobaki; ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu.

7Tena baadhi ya watoto wako mwenyewe wa kiume watapelekwa mateka nao watakuwa matowashi katika ikulu ya mfalme wa Babuloni.”

8Naye Hezekia akamwambia Isaya, “Neno la Mwenyezi-Mungu ulilosema ni sawa.” Alisema hivyo kwani alifikiri, “Kutakuwa na amani na usalama muda wote niishipo.”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help