Yobu 8 - Kiswahili Study Bible

1Ndipo Bildadi, Mshuhi, akamjibu Yobu:

2“Utasema mambo haya mpaka lini?

Mpaka lini maneno yako yatakuwa matupu kama upepo?

3Kwani, wadhani Mungu hupotosha haki?

Au, je, Mungu Mwenye Nguvu hupotosha ukweli?

4Kama watoto wako wamemkosea Mungu,

yeye amewalipiza matokeo ya uhalifu wao.

5Kama utamtafuta Mungu

ukamsihi huyo Mungu mwenye nguvu,

6kama wewe u safi moyoni na mnyofu,

kweli Mungu atakuja kukusaidia,

na kukujalia makao unayostahili.

7Na ingawa ulianza kuishi kwa unyonge

maisha yako ya baadaye yatakuwa ya fahari zaidi.

8Jifunze tafadhali kwa wale waliotutangulia,

zingatia mambo waliyogundua hao wazee.

9Sisi ni watu wa juzijuzi tu, hatujui kitu;

siku zetu duniani ni kivuli kipitacho.

10Lakini wao watakufunza na kukuambia,

mambo waliyopata kuyatoa katika maarifa yao:

11Mafunjo huota tu penye majimaji,

matete hustawi mahali palipo na maji.

12Hata kama yamechanua na bila kukatwa,

yakikosa maji hunyauka kabla ya mimea mingine.

13Ndivyo walivyo wote wanaomsahau Mungu.

Tumaini la wasiomwamini Mungu litapotea.

14Tegemeo lao huvunjikavunjika,

tumaini lao ni utando wa buibui.

15Wanaegemea nyumba yao lakini haitasimama,

huishikilia lakini haidumu.

16Jua litokapo yeye hustawi;

hueneza matawi yake bustanini mwake.

17Mizizi yake hujisokotasokota kwenye mawe

naye aenda kuchunguza ndani ya mwamba.

18Lakini akiangamizwa kutoka makao yake,

hayo yatamkana yakisema: ‘Sijapata kukuona.’

19Tazama, huo ndio mwisho wa furaha ya mtu huyo,

na mahali pao patachipua wengine.

20“Tazama! Mungu hatamkataa mtu asiye na hatia,

wala kuwasaidia waovu.

21Ila atakijaza kinywa chako kicheko,

na midomo yako sauti ya furaha.

22Wale wakuchukiao wataingiwa na aibu,

makao ya waovu yatatoweka kabisa.”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help