Yobu 11 - Kiswahili Study Bible

Hoja ya Sofari

1Kisha Sofari, Mnaamathi, akamjibu Yobu:

2“Je, wingi huu wa maneno uachwe tu bila kujibiwa?

Je, mtu wa maneno mengi aonesha kuwa hana hatia?

3Je, kuropoka kwako kutanyamazisha watu?

Na kama ukidhihaki, je, hamna atakayekuaibisha?

4Wewe wadai: ‘Ninachosema ni kweli,

naam, sina lawama mbele ya Mungu.’

5Laiti Mungu angefungua kinywa chake

akatoa sauti yake kukujibu!

6Angekueleza siri za hekima,

maana yeye ni mwingi wa maarifa.

Jua kwamba Mungu hakuhesabu makosa yako yote.

7“Je, unaweza kugundua siri zake Mungu

na kujua ukomo wake yeye Mungu mwenye nguvu?

8Ukuu wake wapita mbingu, wewe waweza nini?

Kimo chake chapita Kuzimu,

wewe waweza kujua nini?

9Ukuu huo wapita marefu ya dunia,

wapita mapana ya bahari.

10Kama Mungu akipita,

akamfunga mtu na kumhukumu,

nani awezaye kumzuia?

11Mungu anajua watu wasiofaa;

akiona maovu yeye huchukua hatua.

12“Mpumbavu hawezi kuwa na maarifa,

pundamwitu ni pundamwitu tu.

13“Yobu, ukiufanya moyo wako mnyofu,

utainua mikono yako kumwomba Mungu!

14Kama una uovu, utupilie mbali.

Usikubali ubaya uwemo nyumbani mwako.

15Hapo utajitokeza mbele ya watu bila lawama,

utakuwa thabiti bila kuwa na hofu.

16Utazisahau taabu zako zote;

utazikumbuka tu kama mafuriko yaliyopita.

17Maisha yako yatang'aa kuliko jua la adhuhuri,

giza lake litabadilika kuwa mng'ao wa pambazuko.

18Utakuwa na ujasiri maana lipo tumaini;

utalindwa na kupumzika salama.

19Utalala bila kuogopeshwa na mtu;

watu wengi watakuomba msaada.

20Lakini waovu macho yao yatafifia,

njia zote za kutorokea zitawapotea;

tumaini lao la mwisho ni kukata roho!”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help