Zaburi 86 - Kiswahili Study Bible

Kuomba msaada(Sala ya Daudi)

1Unitegee sikio, ee Mwenyezi-Mungu, unijibu,

maana mimi ni fukara na mnyonge.

2Uyahifadhi maisha yangu maana mimi ni mchaji wako;

uniokoe mimi mtumishi wako ninayekutegemea.

3Wewe ni Mungu wangu;

basi, unionee huruma,

maana nakulilia mchana kutwa.

4Uifurahishe roho yangu mimi mtumishi wako,

maana sala zangu nazielekeza kwako ee Bwana.

5Wewe, ee Bwana, u mwema na mwenye kusamehe;

mwingi wa fadhili kwa wote wakuombao.

6Ee Mwenyezi-Mungu, uitegee sikio sala yangu;

ukisikie kilio cha ombi langu.

7Siku za taabu nakuita,

maana wewe waniitikia.

8Ee Bwana, hakuna Mungu aliye kama wewe;

hakuna awezaye kufanya unayofanya wewe.

9Mataifa yote uliyoyaumba, yatakuja kukuabudu, ee Bwana;

yatatangaza ukuu wa jina lako.

10Wewe ndiwe mkuu, wafanya maajabu;

wewe peke yako ndiwe Mungu.

11Unifundishe njia yako, ee Mwenyezi-Mungu,

nipate kuwa mwaminifu kwako;

uongoze moyo wangu nikuheshimu.

12Ee Bwana, Mungu wangu, nitakusifu kwa moyo wote;

nitatangaza ukuu wa jina lako milele.

13Fadhili zako kwangu ni nyingi mno!

Umeniokoa kutoka chini kuzimu.

14Ee Mungu, watu wenye kiburi wamenikabili;

kundi la watu wakatili wanataka kuniua,

wala hawakujali wewe hata kidogo.

15Lakini wewe Bwana, ni Mungu wa rehema na huruma;

wewe ni mvumilivu, mwingi wa fadhili na uaminifu.

16Unigeukie, unihurumie;

unijalie nguvu yako mimi mtumishi wako,

umwokoe mtoto wa mjakazi wako.

17Unioneshe ishara ya wema wako, ee Mwenyezi-Mungu,

ili wale wanaonichukia waaibike,

waonapo umenisaidia na kunifariji.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help