Zaburi 118 - Kiswahili Study Bible

Sala ya shukrani

1Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, kwa kuwa ni mwema,

kwa maana fadhili zake zadumu milele.

2Watu wa Israeli na waseme:

“Fadhili zake zadumu milele.”

3Wazawa wa Aroni na waseme:

“Fadhili zake zadumu milele.”

4Wote wamchao Mwenyezi-Mungu na waseme:

“Fadhili zake zadumu milele.”

5Katika taabu yangu nilimwomba Mwenyezi-Mungu,

naye akanisikia na kuniweka huru.

6Mwenyezi-Mungu yuko nami, siogopi kitu;

binadamu ataweza kunifanya nini?

7Mwenyezi-Mungu yuko nami, kunisaidia;

nami nitawaona maadui zangu wameshindwa.

8Afadhali kukimbilia usalama kwa Mwenyezi-Mungu,

kuliko kumtumainia mwanadamu.

9Afadhali kukimbilia usalama kwa Mwenyezi-Mungu,

kuliko kuwatumainia viongozi wa dunia.

10Mataifa yote yalinizingira,

lakini kwa jina la Mwenyezi-Mungu nikayaangamiza!

11Yalinizunguka kila upande,

lakini kwa jina la Mwenyezi-Mungu, nikayaangamiza!

12Yalinizunguka, mengi kama nyuki,

lakini yakateketea kama kichaka motoni;

kwa jina la Mwenyezi-Mungu niliyaangamiza!

13Nilishambuliwa mno karibu nishindwe,

lakini Mwenyezi-Mungu alinisaidia.

14Mwenyezi-Mungu ni nguvu yangu kuu;

yeye mwenyewe ndiye wokovu wangu.

15Sauti za furaha ya ushindi zasikika hemani mwao waadilifu:

“Mkono wa Mwenyezi-Mungu umetenda mambo makuu!

16Mkono wa nguvu wa Mwenyezi-Mungu umeleta ushindi!

Mkono wa Mwenyezi-Mungu umetenda mambo makuu!”

17Sitakufa, bali nitaishi,

na kusimulia matendo ya Mwenyezi-Mungu.

18Mwenyezi-Mungu ameniadhibu sana,

lakini hakuniacha nife.

19Nifungulie milango ya watu waadilifu,

niingie na kumshukuru Mwenyezi-Mungu!

20Huu ndio mlango wa Mwenyezi-Mungu,

watu waadilifu watapitia humo.

21Nakushukuru, ee Mungu kwa kunijibu;

kwa sababu wewe ni wokovu wangu.

22Jiwe walilokataa waashi,

limekuwa jiwe kuu la msingi.

23Hiyo ni kazi yake Mwenyezi-Mungu

nayo ni ya ajabu sana kwetu.

24Hii ndiyo siku aliyoifanya Mwenyezi-Mungu;

tushangilie na kufurahi.

25Tafadhali utuokoe, ee Mwenyezi-Mungu!

Tafadhali utufanikishe, ee Mwenyezi-Mungu!

26Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Mwenyezi-Mungu!

Twawabariki kutoka nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu

27Mwenyezi-Mungu ni Mungu;

yeye ametujalia mwanga wake

Shikeni matawi ya sherehe,

mkiandamana mpaka madhabahuni.

28Wewe ni Mungu wangu, nami ninakushukuru;

ninakutukuza, ee Mungu wangu.

29Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema,

kwa maana fadhili zake zadumu milele.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help