Zaburi 108 - Kiswahili Study Bible

Sala ya kujikinga na maadui(Zaburi ya Daudi: wimbo)

1Niko thabiti moyoni, ee Mungu,

naam, niko thabiti moyoni;

nitaimba na kukushangilia!

Amka, ee nafsi yangu!

2Amkeni enyi kinubi na zeze!

Nitayaamsha mapambazuko!

3Ee Mwenyezi-Mungu, nitakushukuru kati ya mataifa;

nitakuimbia sifa kati ya mataifa.

4Fadhili zako ni kubwa kuliko mbingu;

uaminifu wako waenea hata mawinguni.

5Utukuzwe, ee Mungu juu ya mbingu!

Utukufu wako uenee duniani kote!

6Watu hao uwapendao na wasalimishwe;

utusaidie kwa mkono wako na kutusikiliza.

7Mungu amesema kutoka patakatifu pake:

“Sasa nitaigawa Shekemu kwa shangwe,

bonde la Sukothi nitalipima sehemusehemu.

8Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu;

Efraimu ni kofia yangu ya chuma,

na Yuda ni fimbo yangu ya enzi.

9Moabu ni kama bakuli langu la kunawia;

kiatu changu nitaitupia Edomu kuimiliki.

Nitapiga kelele ya ushindi juu ya Filistia!”

10Ni nani, atakayenipeleka kwenye mji wa ngome?

Ni nani atakayeniongoza mpaka Edomu?

11Je, umetuacha kabisa, ee Mungu?

Wewe huendi tena na majeshi yetu!

12Utupatie msaada dhidi ya maadui zetu,

maana msaada wa binadamu haufai kitu.

13Mungu akiwa upande wetu tutashinda,

yeye atawaponda maadui zetu.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help