Zaburi 42 - Swahili Common Language DC Bible

KITABU CHA PILI(Zaburi 42–72)Sala ya Mkimbizi(Kwa Mwimbishaji. Utenzi wa Wakorahi)

1Kama paa atamanivyo maji ya kijito,

ndivyo ninavyokutamani, ee Mungu wangu!

2Naona kiu ya Mungu, kiu ya Mungu aliye hai.

Nitafika lini kwake na kuuona uso wake?

3Machozi yamekuwa chakula changu mchana na usiku,

waliponiambia kila siku: “Yuko wapi Mungu Wako!”

4Nakumbuka tena mambo haya

kwa majonzi moyoni mwangu:

Jinsi nilivyokwenda na umati wa watu,

nikawaongoza kwenda nyumbani kwa Mungu

wakipiga vigelegele vya shukrani;

umati wa watu wakifanya sherehe!

5Mbona nasononeka hivyo moyoni?

Kwa nini nahangaika hivyo ndani mwangu?

Nitamtumainia Mungu,

maana nitamsifu tena

yeye aliye msaada wangu na Mungu wangu.

6Nimesongwa na huzuni moyoni mwangu,

kwa hiyo ninakukumbuka wewe, ee Mungu,

kutoka katika eneo la Yordani,

kutoka mlima Hermoni na Mizari.

7Nimeporomoshewa mafuriko ya maji

mafuriko ya maji yaja karibu

nayo yaita maporomoko mapya.

Mawimbi na mapigo yako yamenikumba.

8Mwenyezi-Mungu atanijalia fadhili zake mchana;

nami nimwimbie wimbo wa sifa usiku,

nimwombe Mungu anipaye uhai.

9Namwambia Mungu, mwamba wangu:

“Kwa nini umenisahau?

Yanini niende huko na huko nikiomboleza

kwa kudhulumiwa na adui yangu?”

10Nimepondwa kwa matukano yao,

wanaponiuliza kila siku:

“Yuko wapi, Mungu wako!”

11Mbona nasononeka hivyo moyoni?

Kwa nini nahangaika hivyo?

Nitamtumainia Mungu,

maana nitamsifu tena Mungu,

aliye msaada wangu na Mungu wangu.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help