Yobu 40 - Swahili Common Language DC Bible

1Mwenyezi-Mungu akaendelea kumwambia Yobu:

2“Je, wewe mwenye kuchunguza makosa utashindana na Mungu Mwenye Nguvu?

Wewe unayebishana nami Mungu, basi jibu mambo hayo!”

3Kisha Yobu akamjibu Mwenyezi-Mungu:

4“Mimi sifai kitu nitakujibu nini?

Naufunga mdomo wangu.

5Nilithubutu kusema na sitasema tena.

Nilisisitiza lakini sitaendelea kusema zaidi.”

6Hapo Mwenyezi-Mungu akamjibu kutoka kimbunga:

7“Jikaze kama mwanamume.

Nitakuuliza, nawe utanijibu.

8Je, unataka kweli kubatilisha hukumu yangu,

kuniona nina hatia ili wewe usiwe na hatia?

9Je, una nguvu kama mimi Mungu?

Waweza kunguruma kwa sauti kama yangu?

10“Basi, jioneshe kuwa na fahari na ukuu,

ujipambe kwa utukufu na fahari.

11Wamwagie watu hasira yako kuu;

mwangalie kila mwenye kiburi na kumwangusha.

12Mwangalie kila mwenye kiburi na kumporomosha,

uwakanyage waovu mahali walipo.

13Wazike wote pamoja ardhini;

mfunge kila mmoja kwa kifungo cha kifo.

14Hapo nitakutambua,

kwamba nguvu yako mwenyewe imekupa ushindi.

15“Liangalie lile dude Behemothi,

nililoliumba kama nilivyokuumba wewe.

Hilo hula nyasi kama ng'ombe,

16lakini mwilini lina nguvu ajabu,

na misuli ya tumbo lake ni imara.

17Huufanya mkia wake mgumu kama mwerezi,

mishipa ya mapaja yake imeshonwa pamoja.

18Mifupa yake ni mabomba ya shaba,

viungo vyake ni kama pao za chuma.

19“Hilo ni la kwanza la ajabu kati ya viumbe vyangu!

Ni mimi Muumba wake niwezaye kulishinda.

20Milima wanamocheza wanyama wote wa porini

hutoa chakula chake.

21Hujilaza chini ya vichaka vya miiba,

na kujificha kati ya matete mabwawani.

22Hujisitiri katika vivuli vya vichaka vya miiba

na vya miti iotayo kando ya vijito.

23Mto ukifurika haliogopi,

halitishiki hata mto Yordani ukilifurikia kinywani.

24Nani awezaye kuliziba macho na kuliteka?

Nani awezaye kulitoboa pua kwa mtego?

25 Je, waweza kuvua dude Lewiyathani kwa ndoana,

au kuufunga ulimi wake kwa kamba?

26Je, unaweza kulitia kamba puani mwake,

au kulitoboa taya kwa kulabu?

27Je, wadhani litakusihi uliachilie?

Je, litazungumza nawe kwa upole?

28Je, litafanya mapatano nawe,

ulichukue kuwa mtumishi wako milele?

29Je, utacheza nalo kama ndege,

au kulifunga kamba licheze na wajakazi wako?

30Wadhani wavuvi watashindania bei yake?

Je, wafanyabiashara watathubutu kulikata na kugawana?

31Je, waweza kuichoma ngozi yake kwa mikuki,

au kichwa chake kwa mfumo wa kuvua samaki?

32Jaribu tu kuligusa, uone cha mtema kuni;

Kamwe hutarudia tena kufanya hivyo!

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help