Ufunuo 3 - New Testament: Easy-to-Read Translation

Barua ya Yesu kwa Kanisa la Sardi

1Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi:

Huu ni ujumbe kutoka kwake Yeye mwenye roho saba na nyota saba.

Ninayajua matendo yako. Watu husema kuwa u hai, lakini hakika umekufa.

2Amka! Jitie nguvu kabla ya nguvu kidogo uliyonayo haijakuishia kabisa. Unachofanya hakistahili kwa Mungu wangu.

3Hivyo usisahau kile ulichopokea na kusikia. Ukitii. Geuza moyo na maisha yako! Amka, la sivyo nitakuja kwako na kukushtukiza kama mwizi. Hautajua wakati nitakapokuja.

4Lakini una watu wachache katika kundi lako hapo Sardi waliojiweka safi. Watatembea pamoja nami. Watavaa nguo nyeupe, kwa kuwa wanastahili.

5Kila atakayeshinda atavikwa nguo nyeupe kama wao. Sitayafuta majina yao katika kitabu cha uzima. Nitawakiri mbele za Baba yangu na malaika zake ya kuwa wao ni wangu.

6Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa.

Barua ya Yesu kwa kanisa la Filadelfia

7Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia:

Huu ni ujumbe kutoka kwake aliye mtakatifu na wa kweli, anayeshikilia ufunguo wa Daudi. Anapofungua kitu, hakiwezi kufungwa. Na anapofunga kitu hakiwezi kufunguliwa.

8Ninayajua matendo yako. Nimeweka mbele yako mlango ulio wazi ambao hakuna anayeweza kuufunga. Ninajua wewe ni dhaifu, lakini umeyafuata mafundisho yangu. Hukuogopa kulisema jina langu.

9Sikiliza! Kuna kundi la Shetani. Wanasema kuwa wao ni Wayahudi, lakini ni waongo. Si Wayahudi halisi. Nitawafanya waje mbele yako na kusujudu kwenye miguu yako. Watajua ya kuwa ninakupenda.

10Umeifuata amri yangu kwa uvumilivu. Hivyo nitakulinda wakati wa shida itakayokuja ulimwenguni, wakati ambapo kila aishiye duniani atajaribiwa.

11Naja upesi. Ishikilie imani uliyonayo, ili mtu yeyote asiichukue taji yako.

12Wale watakaoshinda watakuwa nguzo katika hekalu la Mungu wangu. Hawataliacha hekalu la Mungu tena. Nitaandika juu yao jina la Mungu wangu na jina la mji wa Mungu wangu. Mji huo ni Yerusalemu mpya. Unateremka kutoka mbinguni kwa Mungu wangu. Pia nitaandika jina langu jipya juu yao.

13Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa.

Barua ya Yesu kwa Kanisa la Laodikia

14Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia:

Huu ni ujumbe kutoka kwa yeye aliye Amina, shahidi mwaminifu na wa kweli, aliye chanzo cha uumbaji wa Mungu.

15Ninayajua matendo yako. Wewe si moto wala baridi. Ninatamani kama ungekuwa moto au baridi!

16Lakini wewe ni vuguvugu tu, si moto, wala baridi. Hivyo niko tayari kukutema utoke mdomoni mwangu.

17Unasema wewe ni tajiri. Unadhani ya kuwa umekuwa tajiri na huhitaji kitu chochote. Lakini hujui kuwa wewe ni mnyonge, mwenye masikitiko, maskini, asiyeona na uko uchi.

18Ninakushauri ununue dhahabu kutoka kwangu, dhahabu iliyosafishwa katika moto. Kisha utakuwa tajiri. Nakuambia hili: Nunua kwangu mavazi meupe. Ndipo utaweza kuifunika aibu ya uchi wako. Ninakuagiza pia ununue kwangu dawa ya kuweka kwenye macho yako, nawe utaweza kuona.

19Mimi huwasahihisha na kuwaadhibu wale niwapendao. Hivyo onesha kuwa kuishi kwa haki ni muhimu kwako kuliko kitu kingine. Geuzeni mioyo na maisha yenu.

20Niko hapa! Nimesimama mlangoni nabisha hodi. Ikiwa utaisikia sauti yangu na ukaufungua mlango, nitaingia kwako na kula pamoja nawe. Nawe utakula pamoja nami.

21Nitamruhusu kila atakayeshinda kuketi pamoja nami kwenye kiti changu cha enzi. Ilikuwa vivyo hivyo hata kwangu. Nilishinda na kuketi pamoja na Baba yangu kwenye kiti chake cha enzi.

22Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa.”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help