1 Wakorintho 13 - New Testament: Easy-to-Read Translation

Upendo Uwe Dira Yenu

1Ninaweza kusema kwa lugha zingine, za wanadamu au za malaika. Lakini ikiwa sina upendo, mimi ni kengele yenye kelele na tuazi linalolia.

2Ninaweza kuwa na karama ya unabii, ninaweza kuzielewa siri zote na kujua kila kitu kinachopaswa kujulikana, na ninaweza kuwa na imani kuu kiasi cha kuhamisha milima. Lakini pamoja na haya yote, ikiwa sina upendo, mimi ni bure.

3Ninaweza kutoa kila kitu nilichonacho ili niwasaidie wengine na ninaweza hata kuutoa mwili wangu ili niweze kujisifu. Lakini siwezi kupata chochote kwa kufanya haya yote ikiwa sina upendo.

4Upendo huvumilia na ni mwema. Upendo hauna wivu, haujisifu na haujivuni.

5Upendo hauna kiburi, hauna ubinafsi na haukasirishwi kirahisi. Upendo hautunzi orodha ya mambo waliyoukosea.

6Upendo haufurahi wengine wanapokosa, lakini daima hufurahia ukweli.

7Upendo kamwe haukati tamaa kwa watu. Kamwe hauachi kuamini, kamwe haupotezi tumaini na kamwe hauachi kuvumilia.

8Upendo hautakoma. Lakini karama zote hizo zitafikia mwisho, hata karama ya unabii, karama ya kusema kwa lugha zingine na karama ya maarifa.

9Hizi zitakoma kwa sababu maarifa haya na nabii hizi tulizonazo sasa hazijakamilika.

10Lakini ukamilifu utakapokuja, mambo ambayo hayajakamilika yatakoma.

11Nilipokuwa mtoto, nilizungumza kama mtoto, niliwaza kama mtoto, na kufanya mipango kama mtoto. Nilipokuwa mtu mzima, niliziacha njia za kitoto.

12Ndivyo ilivyo hata kwetu. Kwa sasa tunamwona Mungu kwa taswira tu kama ilivyo katika kioo. Lakini, baadaye, tutamwona uso kwa uso. Kwa sasa ninajua sehemu tu, lakini wakati huo nitajua kila kitu, kama ambavyo Mungu amenijua mimi.

13Hivyo mambo haya matatu yanaendelea; imani, tumaini na upendo. Na lililo kuu zaidi ya haya yote ni upendo.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help