Ufunuo 1 - New Testament: Easy-to-Read Translation

Yohana Aeleza Kuhusu Kitabu Hiki

1Huu ni ufunuo kutoka kwa Yesu Kristo, ambao Mungu alimpa ili awaoneshe watumishi wake yale ambayo ni lazima yatokee muda mfupi ujao. Yesu Kristo alimtuma malaika wake ili amwonyeshe Yohana, mtumishi wake,

2ambaye amesema kila kitu alichokiona. Ni ukweli alioambiwa na Yesu Kristo; ni ujumbe kutoka kwa Mungu.

3Ana heri anayesoma maneno ya ujumbe huu kutoka kwa Mungu kwa kupaza sauti na wale wanaousikia ujumbe huu na kuyatendea kazi yaliyoandikwa ndani yake. Wakati uliosalia ni mfupi.

Yohana Ayaandikia Makanisa

4Kutoka kwa Yohana,

Kwenda kwa makanisa saba yaliyo katika Asia:

Neema na amani ziwe kwenu kutoka kwake aliyepo, aliyekuwepo daima na anayekuja; na kutoka katika roho saba zilizoko mbele ya kiti chake cha enzi;

5na kutoka kwa Yesu Kristo aliye shahidi mwaminifu. Aliye wa kwanza miongoni mwa watakaofufuliwa kutoka kwa wafu na ndiye mtawala wa wafalme wote wa dunia.

Yesu ndiye anayetupenda na ametuweka huru na dhambi zetu kwa sadaka ya damu yake.

6Ametufanya sisi kuwa ufalme wake na makuhani wanaomtumikia Mungu, Baba yake. Utukufu na nguvu viwe kwa Yesu milele na milele! Amina.

7Tazama, Yesu anakuja pamoja na mawingu! Kila mtu atamwona, hata wale waliomchoma. Watu wote wa dunia watamwombolezea. Ndiyo, hili litatokea! Amina.

8Bwana Mungu asema, “Mimi ni Alfa na Omega. Mimi ndiye niliyepo, aliyekuwepo na anayekuja. Mimi ni Mwenye Uwezo Wote.”

9Mimi ni Yohana, mwamini mwenzenu. Tuko pamoja katika Yesu na tunashirikiana mambo haya: mateso, ufalme na uvumilivu wenye subira. Nilikuwa katika kisiwa cha Patmo kwa sababu nimekuwa mwaminifu kwa ujumbe wa Mungu na kwa ajili ya kweli ya Yesu.

10Siku ya Bwana, Roho Mtakatifu alinitawala. Nilisikia sauti kuu nyuma yangu iliyosikika kama tarumbeta.

11Ilisema, “Yaandike kwenye kitabu yale unayoyaona na uyatume kwa makanisa saba ya Efeso, Smirna, Pergamo, Thiatira, Sardi, Filadelfia na Laodikia.”

12Niligeuka nyuma nimwone aliyekuwa anazungumza nami. Nilipogeuka, niliona vinara saba vya taa vya dhahabu.

13Nikamwona mmoja katikati ya vinara aliyeonekana kama Mwana wa Mtu. Alikuwa amevaa vazi refu, na mshipi wa dhahabu uliofungwa kuzunguka kifua chake.

14Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu nyeupe kama theluji. Macho yake yalikuwa kama miali ya moto.

15Miguu yake ilikuwa kama shaba ing'aayo inapochomwa katika tanuru. Sauti yake ilikuwa kama kelele za mafuriko ya maji.

16Alikuwa ameshikilia nyota saba katika mkono wake wa kulia. Upanga wenye makali kuwili ulitoka kinywani mwake. Uso wake ulikuwa jua linalong'aa sana mchana.

17Nilipomwona nilianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Aliweka mkono wake wa kulia juu yangu na kusema, “Usiogope! Mimi ni wa kwanza na wa Mwisho.

18Mimi ndiye ninayeishi. Nilikufa, lakini tazama, niko hai milele na milele! Na ninashikilia funguo za mauti na Kuzimu.

19Hivyo andika unachokiona. Yaandike mambo yanayotokea sasa na mambo yatakayotokea baadaye.

20Hii ni maana iliyofichwa ya nyota na vinara saba vya taa vya dhahabu ulivyoviona: Vinara saba ni makanisa saba. Nyota saba ni malaika wa makanisa saba.”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help