1 Petro 5 - New Testament: Easy-to-Read Translation

Kondoo wa Mungu

1Sasa nina jambo la kuwaambia wazee walio katika kundi lenu. Mimi pia ni mzee nami mwenyewe nimeyaona mateso ya Kristo. Na nitashiriki katika utukufu utakaodhihirishwa kwetu. Hivyo ninawasihi,

2mlitunze kundi la watu mnalowajibika kwalo. Ni kundi lake Mungu. Basi lichungeni kwa moyo wa kupenda na si kwa kulazimishwa. Hivi ndivyo Mungu anavyotaka. Fanyeni hivyo kwa sababu mnafurahi kutumika, na si kwa sababu mnataka pesa.

3Msiwaongoze wale mnaowasimamia kwa kuwaamrisha. Lakini muwe mfano mzuri wa kuiga kwao.

4Ili Kristo aliye Mchungaji Mkuu atakapokuja, mpate taji yenye utukufu na isiyopoteza uzuri wake.

5Vijana, nina jambo la kuwaambia ninyi pia. Mnapaswa kutii mamlaka ya wazee. Na ninyi nyote mnapaswa kuwa wanyenyekevu ninyi kwa ninyi.

“Mungu yu kinyume na wanaojivuna,

lakini ni mwema kwa wanyenyekevu.”

6Hivyo mjinyenyekeze chini ya mkono wa Mungu wenye nguvu. Kisha, wakati sahihi utakapofika, atawalipa kwa kuwainua.

7Mpeni Mungu masumbufu yenu yote, kwa sababu Yeye anawajali.

8Iweni na kiasi na muwe waangalifu! Shetani ni adui yenu naye huzunguka zunguka kama simba anayeunguruma akimtafuta yeyote wa kumshambulia na kumla.

9Mpingeni ibilisi. Kisha msimame imara katika imani yenu. Mnafahamu kwamba ndugu zenu ulimwenguni kote wanapitia mateso sawa na hayo mliyonayo.

10Ndiyo, mtateseka kwa muda mfupi. Lakini baada ya hapo, Mungu ataweka kila kitu sawa. Atawatia nguvu, atawasaidia na kuwashika msianguke. Yeye ni Mungu ndiye chanzo cha neema yote. Aliwachagua mshiriki katika utukufu wake ndani ya Kristo. Utukufu huo utadumu milele.

11Uwezo wote ni wake milele. Amina.

Salamu za Mwisho

12Sila ataileta barua hii kwenu. Nafahamu kwamba ni ndugu mwaminifu katika familia ya Mungu. Niliandika barua hii fupi kuwatia moyo na kuwaambia kuwa hii ni neema ya kweli ya Mungu. Simameni imara katika neema hiyo.

13Kanisa lililoko Babeli linatuma salamu kwenu. Wameteuliwa kama ninyi. Marko, ambaye ni kama mwanangu kwangu katika Kristo, anawasalimu pia.

14Mpeni kila mmoja wenu salamu maalumu mnapokutana.

Amani iwe kwenu ninyi nyote mlio katika Kristo.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help