1Salamu kutoka kwa Paulo. Mimi ni mtume kwa sababu Kristo Yesu alinichagua. Alinichagua kwa sababu hivyo ndivyo Mungu alitaka. Naandika barua hii kwa msaada wa Sosthenesi aliye kaka yetu katika Kristo.
2Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, ninyi ambao mmefanywa watakatifu kwa sababu mmeunganishwa kwa Kristo Yesu. Mlichaguliwa kuwa watakatifu wa Mungu pamoja na watu wote kila mahali wanaomwamini Bwana Yesu Kristo, Bwana wao na Bwana wetu.
3Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nanyi.
Paulo Amshukuru Mungu4Ninamshukuru Mungu daima kwa sababu ya neema aliyowapa katika Kristo Yesu.
5Ambaye kwa njia yake Mungu amewabariki sana kwa namna mbalimbali hata miongoni mwenu wapo watu wenye vipawa vya kuzungumza na wengine wana vipawa vya maarifa!
6Hii ni kwa sababu yale tuliyowaambia kuhusu Kristo yamedhihirika kuwa kweli katikati yenu.
7Na sasa mna karama zote mnapomsubiri Mungu audhihirishie ulimwengu jinsi Bwana wetu Yesu Kristo alivyo wa ajabu.
8Ataendelea kuwatia nguvu na hakuna atakayeweza kuwashtaki mpaka siku ya mwisho Bwana wetu Yesu atakaporudi.
9Mungu ni mwaminifu. Na ndiye aliyewachagua ninyi ili mshiriki uzima pamoja na Mwanaye, Yesu Kristo Bwana wetu.
Acheni Mabishano Miongoni Mwenu10Ndugu zangu, kwa mamlaka ya Bwana wetu Yesu Kristo, ninawasihi mpatane ninyi kwa ninyi. Msigawanyike katika makundi. Lakini iweni pamoja tena katika kuwaza kwenu na katika nia zenu.
11Kaka na dada zangu, baadhi ya jamaa wa Kloe wamenitaarifu kuwa kuna mabishano miongoni mwenu.
12Baadhi yenu husema, “Mimi ninamfuata Paulo,” na mwingine husema, “Mimi ninamfuata Apolo.” Mwingine husema, “Mimi ninamfuata Petro,” na mwingine husema, “Mimi ninamfuata Kristo.”
13Kristo hawezi kugawanywa katika makundi. Je! Paulo ndiye alikufa msalabani kwa ajili yenu? Je! mlibatizwa katika jina la Paulo?
14Ninashukuru kwa kuwa sikumbatiza mtu yeyote kwenu isipokuwa Krispo na Gayo.
15Ninashukuru kwa sababu hakuna anayeweza kusema kuwa mlibatizwa katika jina langu.
16(Niliwabatiza pia watu wote wa nyumbani mwa Stefana, lakini sikumbuki kuwa niliwabatiza watu wengine)
17Kristo hakunipa kazi ya kubatiza watu. Alinipa kazi ya kuhubiri Habari Njema pasipo kutumia hekima ya maneno, inayoweza kubatilisha nguvu iliyo katika msalaba wa Kristo.
Nguvu ya Mungu na Hekima Katika Kristo Yesu18Mafundisho kuhusu msalaba yanaonekana ni ya kipuuzi kwao wao wanaoelekea kwenye uharibifu. Lakini ni nguvu ya Mungu kwetu sisi tunaookolewa.
19Kama Maandiko yanavyosema,
“Nitaiharibu hekima ya wenye hekima.
Nitaukanganya uelewa wa wenye akili.”
20Je! hii inasema nini kuhusu mwenye hekima, mtaalamu wa sheria au yeyote katika ulimwengu huu mwenye ujuzi wa kutengeneza hoja zenye nguvu? Mungu ameifanya hekima ya ulimwengu kuwa upuuzi.
21Hii inadhihirisha wazi kuwa, Mungu katika hekima yake aliamua kuwa hawezi kupatikana kwa kutumia hekima ya ulimwengu. Hivyo Mungu aliutumia ujumbe unaoonekana kuwa upuuzi kuwaokoa wale wanaouamini.
22Na hii ndiyo sababu Wayahudi wanataka ishara za miujiza na Wayunani wanataka hekima.
23Lakini ujumbe tunaomwambia kila mtu unahusu Masihi aliyekufa msalabani. Ujumbe huu ni kikwazo kwa Wayahudi na kwa Wayunani ni upuuzi.
24Lakini kwa Wayahudi na Wayunani walioteuliwa na Mungu, Masihi huyu aliyesulibiwa ni nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu.
25Maana upumbavu wa Mungu ni hekima zaidi ya hekima ya kibinadamu, na udhaifu wa Mungu ni nguvu zaidi ya nguvu ya kibinadamu.
26Kaka na dada zangu, fikirini kuhusu hili kwamba Mungu aliwachagua ili muwe milki yake. Wachache wenu mlikuwa na hekima kwa namna dunia inavyoichukulia hekima. Wachache wenu mlikuwa mashuhuri na wachache wenu mnatoka katika familia maarufu.
27Lakini Mungu aliyachagua mambo ambayo wanadamu huyachukulia kuwa ya kipumbavu ili ayaaibishe yenye hekima. Aliyachagua mambo yanayoonekana kuwa manyonge ili ayaaibishe yenye nguvu.
28Aliwachagua wasio kitu ili ayaangamize yale ambayo ulimwengu unadhani ni muhimu.
29Mungu alifanya hivi ili mtu yeyote asisimame mbele zake na akajisifu kuwa yeye ni bora kuliko mwingine.
30Lakini Mungu ameyafungamanisha maisha yenu na Kristo Yesu. Yeye alifanywa kuwa hekima yetu kutoka kwa Mungu. Na kupitia kwake tumehesabiwa haki na Mungu na tumefanywa kuwa watakatifu. Kristo ndiye aliyetuokoa, akatufanya watakatifu na akatuweka huru mbali na dhambi.
31Hivyo, kama Maandiko yanavyosema, “Kila anayejisifu, ajisifu juu ya Bwana tu.”
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.