1 Timotheo 3 - New Testament: Easy-to-Read Translation

Viongozi katika Kanisa

1Usemi huu ni wa kweli kwamba yeyote mwenye nia ya kuhudumu kama mzee, anatamani kazi njema.

2Mzee lazima awe mtu mwema asiyelaumiwa na mtu yeyote. Anapaswa kuwa mwaminifu kwa mke wake. Anapaswa kuwa na kiasi, mwenye busara na mwenye mwenendo mzuri katika maisha, anayeheshimiwa na watu wengine, aliye tayari kuwasaidia watu kwa kuwakaribisha katika nyumba yake. Ni lazima awe mwalimu mzuri.

3Askofu asizoee kunywa mvinyo wala kuwa mgomvi. Bali awe mpole na mtu wa amani, na asiyependa fedha.

4Ni lazima awe kiongozi mzuri kwa familia yake mwenyewe. Hii ina maana kwamba watoto wake wanamtii kwa heshima zote.

5Ikiwa mtu hawezi kuiongoza familia yake mwenyewe, hawezi kulitunza Kanisa la Mungu.

6Ni lazima askofu asiwe yule aliyeamini hivi karibuni. Hii inaweza kumfanya awe na kiburi. Kisha anaweza akahukumiwa kwa kiburi chake kama vile Shetani alivyopanga.

7Pia, ni lazima askofu aheshimiwe na watu walio nje ya Kanisa. Kwa namna hiyo hataweza kukosolewa na kuabishwa na wengine na kunasa kwenye mtego wa Shetani.

Mashemasi

8Kwa njia hiyo hiyo, watu wanaoteuliwa kuwa mashemasi inawapasa kuwa wale wanaostahili kuheshimiwa. Wasiwe watu wanaosema mambo wasiokuwa nayo moyoni au wanaotumia muda wao mwingi katika ulevi. Wasiwe watu wanaowaibia fedha watu wengine kwa udanganyifu.

9Ni lazima waifuate imani ya kweli ambayo Mungu ameiweka wazi kwetu na sikuzote wawe watu wanaotenda mambo yaliyo sahihi.

10Hao unapaswa kuwapima kwanza. Kisha, ukigundua kuwa hawawezi kushitakiwa jambo lolote baya walilotenda, basi wanaweza kuwa mashemasi.

11Kwa njia hiyo hiyo wanawake wanaoteuliwa kuwa mashemasi wanapaswa kuwa wale wanaoastahili kuheshimiwa. Wasiwe wanawake wanaosema mambo mabaya juu ya watu wengine. Ni lazima wawe na kiasi. Ni lazima wawe wanawake wanaoweza kuaminiwa kwa kila jambo.

12Wanaume walio mashemasi lazima wawe waaminifu katika ndoa. Ni lazima wawe viongozi wema wa watoto na familia zao binafsi.

13Mashemasi wanaofanya kazi yao vyema wanajitengenezea nafasi nzuri ya kuheshimiwa. Nao kwa kiasi kikubwa sana wanajihakikishia imani yao katika Kristo Yesu.

Siri ya Maisha Yetu

14Ninatarajia kuja kwenu hivi karibuni. Lakini ninakuandikia maneno haya sasa,

15ili kwamba, hata kama sitakuja mapema, utafahamu jinsi ambavyo watu wanapaswa kuishi katika familia ya Mungu. Familia hiyo ni kanisa la Mungu aliye hai. Na Kanisa la Mungu ni msaada na msingi wa ukweli.

16Ndiyo, Mungu ametuonesha siri ya maisha yanayompa heshima na kumpendeza Yeye. Siri hii ya ajabu ni ukweli ambao wote tunakubaliana nao:

Kristo alijulikana kwetu katika umbile la kibinadamu;

alioneshwa na Roho kuwa kama alivyojitambulisha;

alionwa na malaika.

Ujumbe kuhusu Yeye ulitangazwa kwa mataifa;

watu ulimwenguni walimwamini;

alichukuliwa juu mbinguni katika utukufu.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help