Ufunuo 2 - New Testament: Easy-to-Read Translation

Barua ya Yesu kwa Kanisa la Efeso

1“Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso:

Huu ni ujumbe kutoka kwake yeye anayeshikilia nyota saba katika mkono wake wa kulia na kutembea katikati ya vinara vya taa saba vya dhahabu.

2Ninayajua matendo yako, unavyofanya kazi kwa bidii na usivyokata tamaa. Ninajua kwamba huwakubali watu waovu. Umewajaribu wote wanaojiita mitume lakini si mitume. Umegundua kuwa ni waongo.

3Huachi kujaribu. Umestahimili taabu kwa ajili ya jina langu na hujakata tamaa.

4Lakini nina neno hili nawe umeuacha upendo uliokuwa nao hapo mwanzo.

5Hivyo kumbuka ulipokuwa kabla ya kuanguka. Ugeuze moyo wako na utende yale uliyoyatenda mwanzoni. Usipobadilika, nitakuja kwako na kutoa kinara chako cha taa mahali pake.

6Lakini unafanya vizuri kuyachukia matendo ya Wanikolai. Mimi pia nayachukia mambo wanayotenda.

7Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa. Wale watakaoshinda, nitawapa haki ya kula matunda kutoka kwenye mti wa uzima, ulio katika Bustani ya Mungu.

Barua ya Yesu kwa Kanisa la Smirna

8Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna:

“Huu ni ujumbe kutoka kwake aliye wa Kwanza na wa Mwisho, aliyekufa na akawa hai tena.

9Ninayajua matatizo yako, na ninajua kwamba wewe ni maskini, lakini hakika wewe ni tajiri! Ninayajua matusi unayoteseka kutoka kwa watu wanaojiita Wateule wa Mungu. Lakini si Wayahudi halisi. Watu hao ni wa kundi la Shetani.

10Usiogope mambo yatakayokupata hivi karibuni. Ninakwambia, Ibilisi atawafunga gerezani baadhi yenu ili kuipima imani yenu. Mtateseka kwa siku kumi, lakini iweni waaminifu, hata ikiwa mtatakiwa kufa. Mkiendelea kuwa waaminifu, nitawapa thawabu ya uzima wa milele.

11Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa. Wale watakaoshinda hawatadhuriwa na mauti ya pili.

Barua ya Yesu kwa Kanisa la Pergamo

12Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Pergamo:

Huu ni ujumbe kutoka kwake aliye na upanga wenye makali kuwili unaotoka katika kinywa chake.

13Ninapafahamu mahali unapoishi. Unaishi mahali kilipo kiti cha enzi cha Shetani, lakini wewe ni mwaminifu kwangu. Hukukataa kueleza kuhusu imani yako kwangu hata wakati wa Antipa. Antipa alikuwa shahidi wangu mwaminifu aliyeuawa katika mji wako, mji ambao shetani anaishi.

14Lakini nina vitu vichache kinyume nawe. Una watu huko wanaofuata mafundisho ya Balaamu. Balaamu alimfundisha Balaki namna ya kuwafanya watu wa Israeli kutenda dhambi. Walitenda dhambi kwa kula vyakula vilivyotolewa kwa ajili ya sanamu na kwa kufanya uzinzi.

15Ndivyo ilivyo hata kwa kundi lako. Una watu wanaofuata mafundisho ya Wanikolai.

16Hivyo igeuzeni mioyo yenu! Msipobadilika, nitakuja kwenu haraka na kupigana kinyume na watu hawa kwa kutumia upanga unaotoka katika kinywa changu.

17Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa!

Kila atakayeshinda nitampa mana iliyofichwa. Pia nitampa kila mshindi jiwe jeupe lililoandikwa jina jipya juu yake. Na hakuna atakayejua jina hili isipokuwa yule atakayepata jiwe hili.

Barua ya Yesu kwa Kanisa la Thiatira

18Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira:

Huu ni ujumbe kutoka kwa Mwana wa Mungu, aliye na macho yanayong'aa kama moto na miguu kama shaba inayong'aa.

19Ninayajua matendo yako. Ninajua kuhusu upendo wako, imani yako, huduma yako na uvumilivu wako. Ninajua kwamba unafanya zaidi sasa kuliko ulivyofanya kwanza.

20Lakini ninalo hili kinyume nawe: Umemruhusu yule mwanamke Yezebeli afanye anachotaka. Anasema kwamba yeye ni nabii, lakini anawapotosha watu wangu kwa mafundisho yake. Yezebeli huwaongoza watu wangu kutenda dhambi ya uzinzi na kula vyakula vilivyotolewa kwa sanamu.

21Nimempa muda ili aubadili moyo wake na kuiacha dhambi yake, lakini hataki kubadilika.

22Hivyo nitamtupa kwenye kitanda cha mateso. Na wale wote wanaozini naye watateseka sana. Nitafanya hivi sasa ikiwa hawataacha mambo anayofanya.

23Pia, nitawaua wafuasi wake. Ndipo makanisa yote wataona kuwa mimi ndiye ninayefahamu kile ambacho watu wanadhani na kufikiri. Na nitamlipa kila mmoja wenu kutokana na kile alichotenda.

24Lakini ninyi wengine mlioko Thiatira ambao hamjafuata mafundisho yake. Hamjajifunza mambo yanayoitwa ‘Siri za ndani za Shetani.’ Hivi ndivyo ninawaambia: Sitawatwika mzigo wowote.

25Shikeni katika kweli mliyo nayo tu mpaka nitakapo kuja.

26Nitawapa nguvu juu ya mataifa wale wote watakaoshinda na wakaendelea kutenda yale ninayotaka mpaka mwisho.

27Watayatawala mataifa kwa fimbo ya chuma. Watayavunja vipande vipande kama vyombo vya udongo wa mfinyanzi.

28Watakuwa na nguvu ile ile niliyoipokea kutoka kwa Baba yangu, na nitawapa nyota ya asubuhi.

29Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help